Mfanyabiashara, Mustapha Sabodo amesema atatoa dola za Marekani bilioni 5 (Sh trilioni 10) kwa ajili ya kuwekeza mkoani Dodoma, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kuhamisha makao makuu ya serikali kwenda mkoani humo.

Sabodo amesema atawekeza kiasi hicho cha fedha, iwapo serikali yote itahamia mkoani humo, itakuwa ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitamani kuona mkoa huo unakuwa makao makuu ya nchi.

Pia amesema alichofanya Rais Magufuli, kimewashinda marais wengine waliomtangulia, hivyo yeye kama mfanyabiashara na mtu mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yake, lazima aunge mkono hatua hiyo ya Serikali kuhamia Dodoma ambayo aliita ‘Azimio la Dodoma’.

 Sabodo amesema atatoa fedha hizo ili zitumike kuwekeza kwenye viwanda kama vya mvinyo, viwanda vya kusindika mihogo na viwanda vingine ambavyo vitahitajika katika mkoa huo.

Pia mfanyabiashara huyo amesema kuwepo kwa huduma hizo mkoani Dodoma, kutasaidia kuufanya mji huo kukidhi matakwa ya watumishi wa umma watakaohamia huko.

Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa atafanya uwekezaji mkubwa huo kwa sababu lengo lake ni kuona mji wa Dodoma, unaungana na miji ya jirani kama Mpwapwa, Kondoa na Manyoni ili kutoa fursa ya kupanua huduma mbalimbali katika makao makuu hayo ya nchi.

Sabodo ameema kwamba juhudi zake za kuwekeza katika huduma za jamii kama shule, pia ataziendeleza katika mkoa huo kwa kuhakikisha kwamba zinajengwa shule kadhaa za kisasa, ambazo zitamudu mahitaji ya watu wa eneo hilo.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *