Rais wa chama cha wanasheria nchini, Tundu Lissu leo ameachiwa kwa dhamana katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu jijini Dar es Salaam.
Lissu ambaye anatetewa na Mawakili 18, wakiongozwa na Fatma Karume amepata dhamana kwa kutimiza masharti baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kutupilia mbali ombi la upande wa mashtaka la kumnyima dhamana.
Katika uamuzi huo, Hakimu Mashauri amesema upande wa mashtaka ulishindwa kutaja kesi ambayo Tundu Lissu aliwahi kuruka dhamana.
Aidha, kuhusu kutopewa dhamana kwa ajili ya usalama wake, Hakimu Mashauri amesema sababu hiyo haijitoshelezi kumuweka ndani akisema kundi la Mawakili 18 waliojitokeza kumuwakilisha ni kuonesha upendo wa watu juu yake hivyo kusimama kidete.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri amemuachia kwa dhamana Tundu Lissu kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja alisaini bondi ya Tsh. Milioni 10 huku akitakiwa pia kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.