Rwanda imetangaza kumfukuza kazi kocha wa timu ya taifa ya nnchi hiyo ‘Amavubi’, Jonathan McKinstry kwa matokeo yasiyo ya kuridhisha.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya michezo ya Rwanda imethibitisha kuonyeshwa mlango kwa kocha huyo raia wa Uingereza.

Katibu mkuu wa wizara hiyo, kanali Patrice Rugambwa amesema sababu ya kumfukuza kazi kocha huyo ni matokeo yasiyo ya kuridhisha ya timu ya taifa Amavubi.

Rwanda kwa sasa ni ya tatu katika kundi lake kuwania tiketi ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Afrika la mataifa nchini Gabon mwakani ikiwa na alama 6.

Kundi hili linaongozwa na Ghana, ikifwatiwa na Msumbiji na Mauritius ya mwisho lakini haina tena matumaini ya kufuzu.

Jonathan McKinstry alipewa mkataba wa kuifundisha Amavubi mwaka jana na akaongezewa mwaka huu baada ya kuiwezesha timu hiyo kucheza robo fainali ya mashindano ya CHAN ilipoondolewa na DRC.

Kocha huyo alipoanza kuifundisha timu hiyo ilikuwa katika nafasi ya 68 kwa ubora wa FIFA duniani lakini sasa iko kwenye nafasi ya 121.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *