Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amezungumzia tukio la watu wenye silaha kuvamia nyumbani kwake majira ya mchana na kupambana na vikosi vya usalama.

Watu hao wenye silaha wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Ruto eneo la Sugoi  majira ya saa saba mchana na kwamba baada ya kumzidi nguvu mlinzi aliyekuwa getini waliingia ndani na kupambana na vikosi vya ulinzi kwa kwa takribani saa mbili.

Akizungumzia tukio hilo leo katika uwanja wa Ihura, Ruto amesema watu hao walikuwa na lengo la kuvunja umoja na amani iliyojengeka ndani ya nchi hiyo.

Ruto na familia yake hawakuwa nyumbani wakati tukio hilo la uvamizi lilipotokea. Helkopta ya Polisi ilionekana juu ya eneo la nyumba ya Ruto majira ya saa tisa kasoro na vikosi vya usalama viliwadhibiti watu hao.

Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya kuripotiwa tukio la kundi la Al-shabaab kuteka gari lililokuwa kwenye msafara wa kampeni za Jubilee katika eneo la Mandela, mpakani mwa nchi hiyo na Somalia.

Mkuu wa polisi wa kituo cha Mandela South, Charles Chacha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa juhudi za kuwaokoa watu waliokuwa ndani ya gari hilo zinaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *