Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeanika madudu ya mkataba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye mradi wa Mlimani City.

Madudu hayo yanaonyesha namna chuo hicho kinavyopoteza mamilioni ambako amependekeza mkataba huo ufanyiwe marekebisho.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, ujenzi wa mradi wa Mlimani City ulianza Oktoba Mosi mwaka 2004, ukikadiriwa kukamilika Septemba Mosi mwaka 2016.

Hata hivyo, CAG ameshauri yafanyike marekebisho katika baadhi ya vifungu vya mkataba huo.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba moja ya sababu ya kukiukwa maeneo ya mkataba wa wabia hao wawili ni uzembe wa menejimenti ya chuo.

Ripoti inasema: “Tulibaini kwamba mradi mdogo wa hoteli ya nyota tatu (ambayo ina vyumba 100 kikiwemo chumba cha mikutano kinachochukua watu 1,000) na uboreshaji wa bustani ya botania, ikiwa ni sehemu ya mradi wa Mlimani City, haujakamilika kwa kipindi cha miaka 10 tangu tarehe ya makubaliano ya kumaliza mradi.

“Mtazamo wangu ni kuwa hakuna ufuatiliaji wa karibu, usimamizi na tathmini ya mkataba huo kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kwa sababu hiyo kuna uwezekano wa kushidwa kumalizia kazi iliyobaki kwa sababu ya ongezeko kubwa ya gharama ya kumalizia mradi tangu kipindi kilichopangwa kupita.

“Menejimenti ya Chuo Kikuu inashauriwa kuuangalia upya mkataba iliouingia na Mlimani City Holding, kuharakisha umaliziaji wa miradi,”.

Ripoti hiyo pia inaainisha ukiukwaji wa ulipaji wa ada ambayo mwekezaji anatakiwa kuitoa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Source: Jamii Forum

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *