Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete  amekuwa akiwasiliana na kujuliana hali na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kwa kadiri muda unavyowaruhusu.

Ridhwani amesema hayo baada ya picha zake kusambaa katika mitandao mbalimbali ya jamii zikimwonyesha akisalimiana na Lowassa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Simba na Yanga siku ya Jumamosi.

Ridhiwani amesema picha iliyojengwa kwa baadhi ya wanajamii kuwa baba yake na Lowassa ni maadui, haina ukweli wowote bali ni marafiki na wamekuwa na mawasiliano ya simu na wakati mwingine ya ana kwa ana.

Ridhiwani alisema watu wanapaswa kutenganisha urafiki wa kazi na nje ya kazi.

Amesema nje ya kazi Kikwete na Lowassa ni marafiki, wanawasiliana na kusaidiana na kwamba urafiki wao ndio umewafanya watoto wa familia hizo mbili kuwa huru kwa wazazi wao.

Kuhusu alichoongea na Lowassa alipokwenda kumsalimia walipokutana wakati wa mchezo wa mpira baina ya Simba na Yanga amesema aliitumia pia fursa hiyo kubadilishana naye mawazo kwa sababu alikuwa hajamwona muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *