Klabu ya Real Madrid ya Uhispania imeibamiza Juventus 4-1 na kushinda Kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Cristiano Ronaldo alifunga mabao mawili la kwanza kwake na klabu dakika ya 20 na lake la pili dakika ya 64.

Casemiro aliwafungia Real bao lao la pili dakika ya 61 kabla ya Asensio kukamilisha ushindi wao dakika ya 90 kwa bao lao la nne.

Juventus, waliokuwa wameanza vyema mechi hiyo wakikuwa wamekomboa bao la kwanza la Ronaldo dakika ya 27 kupitia Mario Mandzukic na kufanya mambo kuwa sare wakati wa mapumziko lakini kipindi cha pili mambo yakabadilika.

Mchezaji wa Juve, Juan Cuadrado alipewa kadi ya pili ya manjano dakika ya 84, baada ya kukaa uwanjani dakika 18 pekee.

Gareth Bale aliingia kwenye mechi hiyo kama nguvu mpya, mara yake ya kwanza kuchezeshwa mechi ya ushindani tangu 23 Aprili.

Mechi hiyo iliyochezewa Cardiff ilikuwa ya 19 kwa klabu hizo mbili kukutana, mechi zote zikiwa katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya.

Klabu hizo ndizo zilizokutana mara nyingi kabisa historia ya michuano hiyo, baada ya Bayern dhidi ya Real Madrid (24).

Juventus na Real Madrid, kila mmoja alikuwa ameshinda mechi nane kati ya hizo, mechi mbili zikimalizika kwa sare.

Mechi yao pekee kukutana fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, Real walishinda 1-0 mwaka 1998 kupitia bao la Pedrag Mijatovic.

Juventus walikuwa wameshinda mara mbili pekee kati ya fainali nane walizocheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya. Walishindwa fainali nne walizocheza karibuni zaidi mwaka 1997, 1998, 2003 na 2015.

Real Madrid wamefanikiwa kuwa klabu ya kwanza tangu AC Milan (1989, 1990) kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya misimu miwili mfululizo, na ni mara yao ya 12 kushinda kombe hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *