Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameiagiza Takukuru kufanya uchunguzi dhidi ya mkandarasi Duwi Construction and Engineering Co. Ltd anayetuhumiwa kughushi nyaraka zinazoonesha alijenga barabara ambazo hazimo kwenye orodha ya barabara za mkoa huo.

Katika kikao cha 38 cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha kilichohudhuriwa na Gambo, Mhandisi wa Barabara Mkoa, Edward Amboka ametoa taarifa za hali ya barabara mkoani hapa, alisema wanamfuatilia mkandarasi huyo anayetuhumiwa kughushi nyaraka na kuidanganya bodi ya manunuzi kuwa amejenga barabara kwenye halmashauri nyingine huku akijua si kweli.

Amboka amesema wanashangaa kwa nini mkandarasi huyo aliomba kazi wilayani Monduli mwaka 2015/16 na mchakato wa kuomba kazi ulifanyika na akapewa fursa ya kuendelea na ujenzi huku wajumbe wa zabuni walipaswa kuhakiki kama kweli ana vigezo vinavyostahili pamoja na vifaa.

Amesema mkandarasi huyo alidaiwa kuwasilisha nyaraka zisizo za kweli, ambapo miongoni mwa nyaraka hizo ni zile zinazohusu kazi alizowahi kuzifanya kwenye halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuwa alijenga barabara ya Oldonyosambu – Ngaramtoni, huku akijua barabara hiyo haipo kwenye mtandao wa barabara za mkoa.

Pia ametuhumiwa kughushi logo ya mkoa, akitumia namba AR/RR, badala ya ile inayotambulika mkoani kwa wahusika wa barabara za mkoa, inayoanzia na kumbukumbu namba LGA na kuwasilisha kwenye bodi kazi nyingine, alizowahi kufanya kama kujenga barabara ya Nkoarua-Sing’isi ambayo haipo kwenye mtandao wa barabara kimkoa.

Pia alituhumiwa kughushi saini ya Mhandisi, Gibson Kisanga ambaye awali alikuwa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na mwaka 2013, alihamishiwa wilayani Longido.

Pia aliomba tena kujenga barabara ya Endabashi – Manyara hadi Basuda wilayani Karatu kwa gharama ya Sh milioni 141.1 kwa mwaka 2015/16 na hadi sasa, anaendelea na kazi hiyo kwa kusuasua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *