Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa hana mpango wa kuachia nafasi yake ya uenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Mghwira alitoa msimamo huo baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo na Rais Dk. John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam jana.

Amesema kwa sasa anachokiangalia ni kusimamia shughuli za maendeleo kwa faida ya Watanzania.

Rais Dk. Magufuli alimteua Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, uteuzi ambao ulizua maswali na mshtuko mkubwa katika tasnia ya siasa.

Mjadala mkubwa uliibuka kutokana na cheo alichopewa, kuwa ni tofauti na kile cha ubunge, huku wengine wakienda mbali zaidi huenda kuna usaliti.

Mghwira ambaye katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, aligombea urais kupitia ACT- Wazalendo, sasa atalazimika kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM.

Mbali na hilo, pia atabeba jukumu la kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *