Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Mecky Sadiki amesema Wakala za Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA) ni mzigo kutokana na kushindwa kufanya kazi zake kwa ubora unaokubalika huku ikitoza gharama kubwa za matengenezo ya magari bila sababu za msingi.

Aidha, wakala huo chini ya Wizara ya Ujenzi umedaiwa kutokuwa na mafundi na vipuri stahili vya magari na badala yake imekuwa wakala wa karakana kubwa za magari zinazomilikiwa na watu binafsi.

Sadiki aliyasema hayo wakati akijibu hoja za baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani hapa, walioelezea kutoridhishwa na kazi inayofanywa na Temesa.

Amesema mara kadhaa magari ya serikali yanayopelekwa Temesa hawatengenezi wenyewe ila nao hupeleka katika karakana kubwa zilizopo baadhi ya maeneo mkoani hapa, jambo linaloongeza gharama za matengenezo.

Hata hivyo, amesema ana uhakika wizara ya ujenzi imeiona changamoto hiyo, kwani kinyume na hapo ni kuishushia heshima serikali na kuongeza gharama.

Kauli ya mkuu wa mkoa inafuatia swali la mtumishi wa halmashauri hiyo, John Maimu aliyetaka serikali kuitupia macho Temesa kwa madai inagharama kubwa licha ya kutokuwa na uwezo wa kufanya matengenezo stahili ya magari ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *