Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Bosco Ndunguru, kulipa malimbikizo yote ya mishahara ya miezi 22 yanayofikia Sh 660,000 ya mlinzi wa Shule ya Msingi Ndevelwa, Agustino Paul (58), badala ya kuendelea kumpiga danadana.

Mwanri alitoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Ndevelwa iliyopo katika manispaa hiyo baada ya mkuu huyo wa mkoa kuhutubia wananchi na kutoa nafasi ya kuuliza maswali au kueleza kero zao.

Baada ya mlinzi huyo kutoa malalamiko yake, Mwanri alimwita Mtendaji wa kata hiyo Hamis Kasonta ili kutoa ufafanuzi wa madai hayo, ambapo alikiri mlinzi huyo kutolipwa mishahara yake na uongozi wa shule hiyo ya serikali kwa miezi 22.

Diwani wa kata hiyo, Seleman Maganga, alieleza kuwa awali mlinzi huyo alikuwa anapata mshahara wake kama kawaida, lakini baadaye wakaacha kumlipa kwa kisingizio cha serikali ya kijiji kutopokea fedha yoyote ya uwezeshwaji kutoka halmashauri ya manispaa.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Chatta Lukela, alisema suala hilo lipo chini ya uongozi wa shule na serikali ya kijiji ndio inayopaswa kumlipa mishahara yake yote mlinzi huyo.

Baada ya maelezo hayo, Mwanri alisema kwa kuwa serikali ya kijiji haijapata mgao wa fedha za uwezeshwaji kutoka halmashauri ya manispaa, deni hilo lilipwe moja kwa moja kutoka ofisi ya mkurugenzi wa manispaa na utaratibu wa malipo uanze mara moja hata kama ni kidogo kidogo.

Akizungumza mlinzi huyo amesema alianza kazi hiyo mwaka 2014 kwa makubaliano ya kulipwa Sh 30,000 kwa mwezi na alilipwa miezi kadhaa lakini baada ya hapo hakulipwa tena ila aliambiwa avumilie fedha zikipatikana atalipwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *