Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji amethibitisha rasmi kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti wa klabu hiyo.

Uamuzi huo umekuja muda mfupi tu baada ya Yanga kupata udhamini wa Kampuni ya SportPesa ambayo imesaini mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.

Yanga chini ya Manji imekuwa ikisifika kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa na wenye gharama kubwa kiasi cha kuwazidi nguvu wapinzani wao wa jadi, Simba.

Chini ya Manji, Yanga ilifanikiwa kuwasajili wachezaji kadhaa kutoka Simba ambao walikuwa na majina makubwa wakiwemo Juma Kaseja, Kelvin Yondan, Mganda Emmanuel Okwi na Hassan Kessy.

Manji aliibuka na mkakati wa kuomba kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.

Kutokana na uamuzi huo wa Manji sasa Yanga itakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga akikaimu na nafasi ya mwenyekiti.

Manji ambaye aliingia Yanga mwaka 2006 akiwa mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti amethibitisha kuwa barua iliyosambaa mitandaoni ikiwa na saini yake ni kweli ya kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *