Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amewasili nchini akiwa na mawaziri sita na wafanyabiashara 80.

Afrika Kusini imekubali kutoa mafunzo kwa marubani wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya nchi hizo mbili kuhakikisha Tanzania inakuwa na sekta ya usafirishaji iliyo imara.

Nchi hizo mbili pia zimekubaliana kuhakikisha zinarithisha kwa vizazi vijavyo historia ya ukombozi ambao nchi hizo zilishirikiana katika harakati za kujikwamua kwenye ukoloni ili isije ikapotea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga amesema jana kuwa makubaliano ya kutoa mafunzo kwa marubani wa Tanzania ni sehemu ya mkataba wa uchukuzi ambao nchi hizo zitatiliana saini leo.

Mkataba mwingine ambao utasainiwa leo ni uhifadhi wa mazingira na uoto wa asili. Katika hotuba yake aliyoitoa kwa tume ya marais katika ngazi ya mawaziri kati ya Tanzania na Afrika Kusini, Dk Mahiga alisema mikataba hiyo ina lengo la kuzinufaisha nchi zote mbili ambazo zimekuwa na uhusiano wa kihistoria tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Nkoana Mashabane alisema kuna haja kubwa kwa nchi hizo mbili kuhakikisha historia ya ushirikiano haipotei. Alisema Tanzania imefanya makubwa kwa Afrika Kusini na ndio maana wananchi wa Afrika Kusini wanaona Tanzania ni nyumbani.

Mikataba hiyo itasainiwa leo wakati wa mkutano wa Rais John Magufuli na Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye amewasili jana kwa ziara ya kiserikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *