Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma amempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge).

Zuma ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo rasmi na alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini kupitia vyombo vya habari Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Zuma amesema anatambua kuwa ujenzi wa reli ya kati utaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi za maziwa makuu na hivyo amekubali ombi la Rais Magufuli la kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika ya Kusini kushirikiana na Tanzania kufanikisha mradi huo mkubwa.

Kabla ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari  Rais Magufuli na Zuma wameshuhudia utiaji saini wa hati tatu za ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais Zuma kwa kuitikia mwaliko wake na kukubali kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano na uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania.

Rais Magufuli amesema hivi sasa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini kwa mwaka ni Shilingi Trilioni 2.4, uwekezaji wa Afrika Kusini hapa nchini ni Dola za Marekani Milioni 803.15 uliozalisha ajira 20,916 na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi endapo ushirikiano utaimarishwa zaidi.

Magufuli ameongeza kuwa Tanzania itapeleka walimu wa lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na watu takribani milioni 120 ili wakafundishe lugha hiyo katika vyuo vya Afrika ya Kusini na hivyo kuimarisha zaidi ushirikiano.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *