Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan anatarajia kufanya ziara ya siku mbili nchini kuanzia tarehe 22 na 23 Januari mwaka huu.

Rais Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na atapokelewa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje, Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara  na uwekezaji.

Wakati wa ziara hiyo, Rais Erdogan  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *