Rais wa Shirikisho la Soka dunia (FIFA), Gianni Infantino amezindua ujenzi wa Hoteli ya chama cha soka cha Rwanda kwa gharama za FIFA.

Infantino ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Hoteli hiyo inayojengwa mjini Kigali karibu na uwanja wa taifa Amahoro.

FIFA tayari imeshatoa kitita cha dolla za Marekani milioni 4,1 kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli hiyo huku zikiwa zimesalia dolla milioni 2.

Mwenyekiti wa chama cha soka cha Rwanda FERWAFA, Nzamwita De Gaule amesema Hoteli hiyo itatumiwa kupokea timu mbali mbali kutoka ng’ambo zinazokwenda kucheza nchini Rwanda.

Kwa upande wake Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema aliidhinisha kugharamia mradi wa ujenzi wa Hoteli hii kwa sababu aliutambua kama mradi mzuri wa kusaidia chama cha soka cha Rwanda kwa sababu una malengo mazuri ya kuendeleza soka ambayo pia ndiyo malengo yake.

FIFA itakuwa na mkutano wa kamati tendaji mwezi wa 10 mwaka huu nje ya makao yake mjini Zurich,na Rwanda tayari imekwishaomba kuwa mwenyeji wa mkutano huo.