Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli jana amewapokea marais wawili, Edgar Lungu wa Zambia aliyewasili kwa ziara ya kiserikali na Idriss Deby wa Chad aliyekuja kikazi.

Ujio wa Rais wa Chad ulikuwa wa ghafla na hata serikali ilitoa taarifa ya ujio wake jana saa chache kabla ya kuwasili nchini kiongozi huyo ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Wote wawili baada ya kuwasili nchini walipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride na ngoma za asili.

Licha ya kupokelewa na Rais Magufuli, viongozi wengine waandamizi wa Serikali pia walishiriki kwenye mapokezi ya viongozi hao.

Ratiba ya ziara yao inaonesha kuwa kila mmoja atafanya mazungumzo na Rais Magufuli katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Shughuli za Lungu Ratiba ya Rais Lungu inaonesha leo asubuhi atatembelea ofisi za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo la ubia baina ya nchi hizo.

Baadaye atazuru pia Shirika la Bomba la Mafuta la Tazama, ambapo atatembelea mitambo ya kusukuma mafuta, pamoja na matangi ya kuhifadhi mafuta ya Tazama vyote vilivyopo eneo la Kigamboni. Baada ya ziara hizo za asubuhi, Lungu na ujumbe wake watafanya mazungumzo rasmi na Rais Magufuli, pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *