Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa anatamani msanii wa muziki, Harmonize kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara.

Rais Magufuli amesema hayo katika mkutano wa hadhara mara baada ya msanii huyo kutumbuiza katika mkutano huo uliofanyika mkoani Lindi.

Harmonize amekuwa akikaribishwa kutumbuiza katika mikutano mbalimbali ya hadhara inayofanya na Rais Magufuli mara baada ya kutoa wimbo wake wa Magufuli ambao unaelezea jinsi Rais huyo alivyofanya katika sekta.

Wimbo huo wa Magufuli ulioimbwa kwa mdundo wa nyimbo yake ya zamani ya kwangaru, umemsifu Magufuli kwa kazi aliyoifanya katika uongozi wake.

Iwapo Harmonise atagombea wadhfa huo wa ubunge basi anaweza kuwa msanii wa kwanza maarufu kuchukua kiti cha ubunge kupitia chama tawala.

Kwa Tanzania mwanamuziki kuwa kiongozi sio jambo geni kwani tayari kuna viongozi ambao ni wabunge ingawa wote wanatokea chama cha upinzani.

Msanii wa bongofleva Joseph Haule maarufu kwa jina ‘Profesa Jay’ alipata ubunge wa jimbo la Mikumi mkoani Morogoro tangu mwaka 2015 mpaka sasa.

Profesa Jay alipata wadhfa huo baada ya kutoa wimbo wake uliotamba wa ‘Ndio mzee’ambao ulikuwa unaeleza namna kiongozi anaweza kutoa ahadi bila kuzitimiza.

Msanii mwingine maarufu nchini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu amekuwa mbunge wa Mbeya mjini kupitia chama cha upinzani cha Chadema nchini tangu mwaka 2010 mpaka sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *