Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kesho anatarajia kukabidhi uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni baada kuongoza kwa vipindi viwili.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga katika Mkutano wa 34 wa Baraza la Mawaziri la EAC.

Amesema kuwa Rais Magufuli atakabidhi uenyekiti huo kwa Rais Museveni kwenye mkutano wa viongozi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika kesho.

Balozi Mahiga ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi ambacho Tanzania iliiongoza jumuiya hiyo, ikiwemo kuridhia maombi ya muda mrefu ya uanachama, ya nchi ya Jamhuri ya Sudan Kusini na kuipatia uanachama kamili wa jumuiya hiyo.

Kuhusu mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC uliofanyika jana, alisema wajumbe wa baraza hilo watajadili ushirikiano wa masuala mbalimbali yanayohusu jumuiya hiyo.

Ameongeza kwa kusema kuwa wajumbe hao watajadili namna ya kuondoa na au kupunguza vikwazo visivyo vya kisheria hasa vinavyokwamisha biashara ikiwemo ushuru wa forodha, vizuizi vya magari au kuzuia uzito wa magari au aina fulani za biashara, na kwamba watajadili namna ya kuanzisha soko imara la pamoja.

Pia amesema kuwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa anatarajiwa pia katika mkutano huo kuwasilisha ripoti ya mazungumzo ya pamoja ya kuleta amani, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la wakuu wa nchi wa EAC lililotolewa mwezi Januari,2017.

Marais karibia wote watakuwepo Rais wa Kenya atakuwepo, Rais wa Uganda, Burundi, Rais Kagame atakuja, lakini Sudan wamesema wanahudhuru watatuma mwakilishi tu kwenye mktano huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *