Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya watu waliouziwa mashamba makubwa Mkoani Tanga na kisha kuyatelekeza ambapo mpaka sasa hati miliki za ardhi 5 zenye zaidi ya ekari 14,000 zimefutwa.

Rais Magufuli amesema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mkata, Komkonga, Kabuku, Michungwani, Hale, Muheza na Pongwe katika Wilaya za Handeni, Muheza na Tanga ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku 5 Mkoani wa Tanga.

Rais Magufuli alifafanua kuwa Mkoa wa Tanga una mashamba 72 yaliyouzwa kwa watu mbalimbali na kwamba hatua za kunyang’anya mashamba yaliyotelekezwa zimeanza kuchukuliwa kwa mashamba 12 na tayari mashamba 5 ambayo hati zake zimeshafutwa, utaratibu unaendelea kuwagawia wananchi na wawekezaji watakaokuwa tayari kuyaendeleza kama ilivyokusudiwa.

Sambamba na hilo akiwa Mkata Wilayani Handeni, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza shamba la ekari 50 lililopo katika kijiji cha Kabuku na ambalo lililotolewa na wananchi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa lengo la kujenga kiwanda miaka 7 iliyopita, lirejeshwe kwa wananchi na ametaka JKT ijenge kiwanda hicho katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 9,000.

Rais Magufuli ametoa siku 15 kufanyika kwa uchunguzi wa fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kituo cha afya cha Mkata, kufuatia kuwepo kwa taarifa za ufujaji wa fedha hizo na ameongeza kuwa Serikali itapeleka Shilingi Milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza kituo hicho baada ya hatua stahiki kuchukuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *