Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli leo anatarajiwa kupokea ripoti ya kamati maalum aliyoundwa kuchunguza mchanga ulio katika makontena ya mchanga wa madini.

Tukio hilo litafanyika ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, huku likirushwa moja kwa moja na vituo vya redio, televisheni na tovuti rasmi ya ikulu.

Tukio hilo linatarajiwa kufanyika leo kuanzia saa 3:30 asubuhi katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine Rais Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara wawekezaji wa kutoka Shirikisho la Mitambo ya Viwanda la China (China National Machinery Industry Federation – CNMIF) kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawapa ushirikiano wa kutosha katika mpango wao wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa nishati ya umeme, viwanda na kilimo hapa nchini.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa CNMIF na Mbunge wa Bunge la Wananchi wa China, Zhan Xin.

Rais Magufuli alisema Tanzania imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Megawatts kati ya 1,500 na 1,800 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia Megawatts 10,000 na kwamba ili kufikia malengo hayo wawekezaji wanakaribishwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vilivyopo kama vile gesi, makaa ya mawe na jua.

Katika tukio lingine, Rais Magufuli alikutana na Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak ambapo viongozi hao wamezungumzia utekelezaji wa mambo mbalimbali ya ushirikiano pamoja na miradi ya maendeleo iliyotokana na makubaliano ya Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Ufaransa uliofanyika hivi karibuni.

Viongozi wengine ambao jana walikutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli ni Kaimu Balozi wa Uturuki nchini, Yunus Belet na Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Korea, Songwon Shin.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *