Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amewaongoza Watanzania katika kilele cha maadhimisho ya Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki sherehe hizo.

 Kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni “Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu.”

Maadhimisho hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza tangu Dk Magufuli kuingia madarakani kutokana na mwaka jana kuzisitisha na kutaka kuadhimishwa kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.

Rais Magufuli aliagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa maadhimisho hayo zaidi ya Sh bilioni nne kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.

Katika maadhimisho hayo yatahudhuriwa na marais wa nchi jirani na viongozi wastaafu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema wiki hii kwamba sherehe hizo zitapambwa gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.

Pia kutakuwa na maonesho ya kwata la kimya kimya pamoja na makomandoo wa JWTZ, burudani za vikundi vya muziki wa kizazi kipya na kizazi cha zamani pamoja na ngoma za asili kutoka mikoa ya Mbeya, Pwani, Lindi na Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *