Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, John Pombe Magufuli ametishia kufunga migodi yote inayomilikiwa na makampuni ya nje ikiwa makampuni hayo yatasshindwa kuanzisha mazungumzo haraka juu ya umiliki wao pamoja na tozo wanazopaswa kulipa.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara katika wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambapo yupo kwa ziara ya siku tatu.

Amesema haiwezekani makampuni hayo yanaendelea kuwa kimya wakati wameshakubaliana kuanzisha mazungumzo haraka.

Katika Mkutano huo Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kuwa ataendelea kupambana na kodi zenye kuwakera wananchi hasa wananchi wa hali ya chini.

Amesema mpaka sasa serikali imeondoa kodi katika kilimo na mazao takribani 80 ambazo zilikuwa kero kwa wakulima na itaendelea kuzipunguza mpaka wakulima wafaidike na kilimo hicho.

Kwa muda mrefu wakulima vijijini wamekuwa wakipata usumbufu wakati wa kusafirisha na kuuza mazao yao kwa kubambikiwa kodi nyingi. Hali hii inawarudisha nyuma wakulima badala ya kufaidika wanazidi kuwa masikini kwa kupoteza nguvu nyingi lakini hakuna wanachokipata.

Tangazo hilo toka kwa Rais wao limekuwa faraja na mkombozi mkubwa kwa wakulima wengi pamoja na wafugaji ambao Rais Magufuli amesema imefikia wafugaji walikuwa wanalipa kodi ya kwato kwa maana ya kila kwato ilikuwa ikilipiwa kodi.

Akiwa njiani kutoka Wilayani Kibondo kuelekea Wilaya ya Kasulu, Rais Magufuli alilazimika kusimama njiani kuzungumza na wananchi waliojazana kutaka kumsikiliza. Aliwaambia kuwa maamuzi aliyoyafikia naa kutangaza jana kuwa wakimbizi warudi nyumbani kwao kwa kuwa kuna amani sio kwamba anawafukuza bali ni ukweli kuwa wakimbizi wanachukua asilimia kubwa ya bajeti ya serikali katika mkoa huo.

Akaongeza kuwa yeye hakuchaguliwa na Watanzania kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi wa Burundi bali amechaguliwa na mamilioni ya watanzania kwa ajili ya kuwaletea maendeleo watanzania na nchi yao kwa ujumla.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *