Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchukua hatua wanapokuwa na ushahidi dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo  jana alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa TAKUKURU katika ofisi za makao makuu ya taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.

Pia Rais Magufuli amesema ana imani na TAKUKURU na amewataka wafanyakazi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uzalendo na uadilifu mkubwa na kwamba Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili.

Katika mkutano huo Rais Magufuli amepokea masuala mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa TAKUKURU na amewaahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi ili kuboresha maslahi yao na mazingira ya kazi.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Katibu Mkuu Dkt. Laurian Ndumbaro na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Valentino Mlowola.

Katika Mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Matogolo Kalemani ametoa taarifa ya maandalizi ya awali ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’ Gorge na kwamba zabuni ya kuanza kwa ujenzi huo itatangazwa tarehe 30 Agosti, 2017.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *