Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara, viongozi na wawekezaji, wanaohodhi ardhi bila kuiendeleza na kuwataka waendeleze maeneo hayo ndani ya kipindi hicho, vinginevyo atatumia mamlaka yake kuwanyang’anya ardhi hiyo.

Magufuli amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwaunga mkono na kuwatengenezea mazingira mazuri ya uwekezaji wafanyabiashara wote watakaowekeza kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.

Rais Magufuli amesema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 Kifungu Namba Nne na Tano, kinampatia mamlaka Rais kumnyang’anya mtu yeyote ardhi asiyeitumia kwa mujibu wa sheria na kumpatia mwingine ili aiendeleze.

Amesema hayo katika kijiji cha Mwandege wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani wakati akizindua kiwanda cha kusindika matunda kilichopo chini ya Kampuni ya Food Products mali ya Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) ya Dar es Salaam.

Kuhusu maendeleo ya viwanda nchini, alisema katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2020, umeainisha wazi nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuijenga Tanzania ya Viwanda na kuwataka wawekezaji wakiwemo wazalendo kutumia fursa hiyo.

Pia amesema lengo la serikali ni kuhakikisha sekta ya viwanda inachangia kwenye Pato la Taifa asilimia 15 kutoka asilimia 7.3 ya sasa ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa asilimia 40.

Ametumia fursa hiyo kuwahimiza hata wale waliopata fedha zao isivyo kihalali kuzitumia fedha hizo kwa kuwekeza kwenye viwanda badala ya kuzificha kwa kuzifukia ambapo matokeo yake ni fedha hizo kupoteza uhalali wake wa kutumika.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *