Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo amewachimba mkwara baadhi ya wabunge ambao huwa wanakazi ya kuropoka bungeni na kusema anawasubiri waropoke tena nje ya bunge ili adili nao vizuri kwani wamekuwa wakirudisha watu nyuma katika vita ya uchumi.

Magufuli amesema hayo leo wakati akipokea ripoti ya pili iliyounda kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa madini kwenye makontena ya mchanga ambayo yanafahamika kama Makinikia.

Pia Rais ameahidi kuwa sheria zote za madini zinapaswa kupitiwa tena na kurekebishwa na bunge ili ziweze kuleta tija kwa Watanzania.

Mbali na hilo Rais Magufuli alikubaliana na mapendekezo yote 20 ambayo yameletwa na Kamati hiyo maalum chini Mwenyekiti Prof. Nehemiah Eliachim Osoro ikiwa ni pamoja na baadhi ya Mawaziri pamoja na viongozi wote waliohusika katika kusaini mikataba hiyo kutafutwa popote walipo na kuhojiwa na vyombo vya dola.

Rais Magufuli alikwenda mbali zaidi na kusema Tanzania kuna watu wanakosa madawa katika hospitali, huku akisema watu wengine wanakosa pembejeo mashambani kwa kuwa nchi ni masikini ili hali nchi ina utajiri mkubwa, ambao umekuwa ukitumika vibaya kutokana na tamaa za viongozi ambao siyo wazalendo, viongozi ambao hawajali maslahi ya Watanzania zaidi ya kuangalia maisha yao tu.

Katika hatua nyingine Spika wa Bunge Job Ndugai amekiri kuwa wao kama Bunge wapo tayari kupitia sheria zote zitakazokuja bungeni kwa umakini zaidi ili kuweza kurekebisha mikataba hiyo mibovu iliyoliingizia taifa hasara kubwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *