Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaalika wafanyabiashara wa Cuba na Serikali ya nchi hiyo kuja hapa nchini kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu.

Rais Magufuli ametoa mwaliko huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Lopez Tormo.

Dk. Magufuli amemhakikishia Balozi Jorge Lopez Tormo kuwa Serikali yake itatoa ushirikiano wa kutosha endapo mfanyabiashara yeyote wa Cuba au Serikali yenyewe ya Cuba itajitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na utengenezaji wa dawa za binadamu.

Pia Rais Magufuli amesema Serikali ipo tayari kutoa ardhi kwa mwekezaji yeyote kutoka Cuba atakayekuwa tayari kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu na vifaa tiba hapa nchini.

Kwa upande wake Balozi Jorge Lopez Tormo amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya katika uendeshaji wa Serikali na amemhakikishia kuwa Cuba itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *