Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ameteua wakuu wa wilaya wawili na wakurugenzi 3 wa mamlaka za Serikali za Mitaa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli amemteua Kisare Makori kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Humphrey Polepole ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi.

Mwanasheria maarufu Evod Mmanda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara iliyopo katika Mkoa wa Mtwara. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Khatib Kazungu ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Katika uteuzi huo, Rais Magufuli alimteua Ramadhan Mwangulumbi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga iliyopo mkoani Shinyanga.

Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Lewis Kalinjuna ambaye anastaafu kwa mujibu wa Sheria. Rojas Romuli ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda iliyopo katika Mkoa wa Katavi. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ngalinda Ahmada aliyefariki dunia hivi karibuni.

Mwingine aliyeteuliwa ni Rashid Gembe kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga iliyopo katika Mkoa wa Tanga, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mkumbo Barnabas ambaye uteuzi wake ulitenguliwa hivi karibuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *