Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema atakayethubutu kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar atavunjika yeye kabla ya Muungano.

Akizungumza katika hotuba fupi ya dakika 17 jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ambako sherehe za Muungano zimefanyika kwa mara ya kwanza tangu Uhuru.

Rais Magufuli amesema kuwa kufikisha umri wa miaka 53 ya kuzaliwa kwa taifa la Tanzania si jambo dogo, kwani mataifa mengi yamejaribu kufanya hivyo, lakini bila ya kufanikiwa, huku akisisitiza kwa kusema,”Hii ni siku ya kipekee, ya kihistoria kwa tanzania.

Pia aliongeza kuwa, si jambo dogo kusherehekea Miaka 53 ya Muungano, kwani kazi ya kuulinda Muungano ni ngumu, hivyo basi hatuna budi kuwapongeza waliofanikisha nchi yetu kufikisha miaka 53, tunawapongeza sana.

Rais Magufuli aliendelea kusema kuwa yeye na Dk Shein, watafuata nyayo za kuulinda na kuutetea Muungano huo.

Aidha, alisema wakati Watanzania wakisherehekea kutimiza miaka 53 ya kuzaliwa kwa taifa la Tanzania, ni vyema watu kutafakari walikotoka, walipo na wanakokwenda.

Mwisho alisema anafahamu kukiwa na mshikamano, itawezekana kuulinda Muungano, hivyo kushauri Watanzania wazidi kushikamana ili kuwe na miaka mingine mingi zaidi ya kusherehekea Muungano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *