Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana alimualika Nay wa Mitego Ikulu baada kuachiwa na Jeshi la POlisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Nay wa Mitego jana alikiri kupata mwaliko huo na kueleza kwamba atakapokutana naye, ataitumia nafasi hiyo kumueleza mheshimiwa rais hali halisi ya maisha ya Watanzania kwasasa.

Nay alisema kuwa “Nimepokea mwaliko bado nafikiria nini cha kuongea naye endapo nitapata hiyo nafasi ya kuzungumza naye, nadhani itakuwa nafasi nzuri ya kumweleza vile ambavyo Watanzania sisi tunaishi mtaani,”.

Nay alikamatwa na polisi mkoani Morogoro usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa kile kilichodaiwa kutunga na kutoa wimbo wenye maudhui yanayoikashifu serikali.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe alisema Rais Magufuli ameagiza msanii huyo aachiwe huru na wimbo wake uendelee kuchezwa na kusambazwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *