Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amemtumbua Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru na nafasi yake kurithiwa na Dk. Osward Mashindano.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana usiku, ilieleza kuwa Dk. Mashindano anachukua nafasi hiyo na Mafuru atapangiwa kazi nyingine.

Mafuru, hivi karibuni aliibuka na kauli tata ambayo ilionekana kupingana na Rais Magufuli kuhusu uamuzi wa baadhi ya taasisi za umma kuweka fedha katika Fixed Deposit Accounts (akaunti maalumu).

Kauli hiyo aliitoa Novemba 30, mwaka huu katika mahojiano maalumu na redio moja nchini. Alisema haiwezekani kwa watumishi wa umma kuiba fedha zinazowekwa katika Fixed Deposit Accounts kwa sababu miamala ya benki ni ya uwazi.

Amesema hizo ni tuhuma tu na Serikali imemwagiza CAG kuchunguza.

Amesema hakuna kosa kwa taasisi za Serikali kuweka fedha katika akaunti hizo, lakini Serikali sasa imeamua kuzihamishia Benki Kuu (BoT) ili iwe rahisi kuzifuatilia.

Kauli hiyo ya Mafuru ilitanguliwa na ile ya Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, ambaye alisema si kosa kisheria kwa taasisi kufungua akaunti maalumu katika benki ya biashara.

Novemba 26, mwaka huu, Rais Magufuli alifichua siri ya hatua yake ya kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya bodi hiyo kuidhinisha Sh bilioni 26 kupelekwa kuwekwa katika akaunti maalumu (Fixed Account) katika benki kadhaa za biashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *