Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli leo amezindua mradi wa mabasi yaendao haraka Dar es Salaam (UDART) kwenye hafla ya iliyofanyika Kariakoo, Gerezani.

Rais Magufuli amesema mkandarasi wa kwanza wa Mradi wa Mwendokasi alikuwa Mchina, alishindwa akatumbuliwa akaondoka ndipo akaletwa Strasburg wa Ujerumani.

Pia awaagiza Mawaziri George Simbachawene wa TAMISEMI na Prof. Makame Mbarawa wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na wasimamizi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dara, kufikia leo jioni wampe ripoti inayoonesha kiasi cha fedha iliyopatikana kama faida kwenye mradi huo.

Vile vile amependekeza kujengwa kwa kituo kikubwa cha maegesho ya magari ya daradala na madogo madogo eneo la Kimara ili kuvutia watu ambao wakishuka kwenye magari yao binafsi ama daladala wapande ya mwendokasi, au wakishuka mabasi ya mwendokasi iwe rahisi kupanda daladala au magari yao binafsi.

Rais Magufuli awaagiza vikosi vya Usalama Barabarani kuwashughulikia wanaoingiza magari kwenye njia za mwendokasi kwani wanavunja sheria za nchi. Ameagiza wakamatwe na kupelekwa vituo vya polisi ama kung’oa mataili kwenye magari yao ili liwe fundisho kwao na kwa wengine.

Sherehe hiyo ya uzinduzi imehudhuriwa na viongozi mbali mbali kama vile mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), George Simbachawene.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *