Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Limited kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.

Kiwanda hicho kikubwa Afrika Mashariki na Kati ambacho ujenzi wake umegharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku, kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000.

Baada ya kuweka jiwe hilo la msingi, Rais Magufuli ameishukuru Menejimenti ya kiwanda hicho kwa uwekezaji huo na ameelezea kufurahishwa kwake na kutumika kwa teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema pamoja na kiwanda hicho, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani jumla ya viwanda 2,169 vinavyojumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na vipo katika hatua mbalimbali za kukamilika.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia mkazo juhudi za kukuza uchumi zilizowezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa Barani Afrika na amebainisha kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza uwekezaji nchini Tanzania ikiwemo kujenga viwanda.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *