Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa kutoa mkopo wa bilioni 110 kwa ajili ya kujenga barabara ya Chaya – Nyahua mkoani Tabora yenye urefu wa kilometa 85.

Rais Magufuli alitoa shukrani hiyo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam, alipofanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait hapa nchini, Jasem Ibrahim Al Najem na kupokea msaada wa magari mawili ya kusombea taka ngumu yenye thamani ya Dola za Marekani 200,000.

Magari hayo yametolewa na Serikali ya Kuwait kwa lengo la kuunga mkono kampeni ya usafi hapa nchini.

Rais Magufuli pia aliishukuru Serikali ya Kuwait kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za utoaji wa huduma za kijamii nchini, ikiwemo msaada wa Dola za Marekani 250,000 kwa ajili ya kununulia vifaa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na visima vya maji safi 27 vilivyochimbwa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya wanafunzi na wananchi wa maeneo jirani na shule.

Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya Kuwait kwa kutoa Dola za Marekani milioni 50 kwa ajili ya kuikarabati Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar.

Pia aliiomba Serikali ya Kuwait kuweka alama ya kumbukumbu ya uhusiano wake na Tanzania kwa kusaidia ujenzi wa barabara za makao makuu ya nchi mjini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *