Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Chato alikosoma darasa la kwanza hadi la saba na kuzungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Magufuli pia ameahidi kujenga madarasa matatu na ofisi moja ya walimu katika shule hiyo, kufuatia ombi la walimu kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana, ilieleza kuwa Rais alifanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo.
Akizungumza na wanafunzi shuleni hapo, Magufuli aliwaasa kutilia mkazo masomo ili waweze kufaulu na kuwataka walimu kuhakikisha wanatumia vyema fedha zinazotolewa na serikali kila mwezi za elimu bila malipo na pasiwe na wanafunzi hewa.
Rais amesema yapo maeneo na shule mbalimbali nchini kumebainika kuwa na wanafunzi hewa katika uhakiki unaofanywa na serikali na kuwaasa shule hiyo kuwa wasiwe kama shule hizo.