Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana amefanya ziara katika bandari ya Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo Rais Magufuli ameshuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi tarehe 02 Machi, 2017.

Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP – Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa popote ulipo, mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.

Akiwa bandarini hapo Mhe. Dkt. Magufuli pia ameshuhudia udanganyifu mwingine unaofanywa na wafanyabiashara wanaoagiza mizigo kutoka nje ya nchi baada ya kuoneshwa makontena ambayo nyaraka zinaonesha yamebeba mitumba ya nguo na viatu wakati ndani yake kila kontena moja limebeba magari matatu ya kifahari.

Kwa upande wa Maafisa wa bandari ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kufuatia maelekezo aliyoyatoa ya kuhakikisha mizigo yote inakaguliwa kwa mitambo ya mionzi (Scanning Machines) wamefanikiwa kubaini udanganyifu mwingi unaofanywa na wafanyabiashara wanaoingiza nchini na kusafirisha nje ya nchi mizigo mbalimbali yakiwemo makontena 10 ambayo yamepatikana yakiwa na magari ya kifahari ilihali nyaraka zake zikionesha yana mitumba ya nguo na viatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *