Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ameagiza eneo la ekari 50 lililopo Mkata mkoani Tanga ambalo walipewa Mgambo JKT kurudishwa kwa serikali ya kijiji.

JKT Mgambo walipewa shamba hilo miaka saba iliyopita kwa ajili ya kujenga kiwanda na wakashindwa kuliendeleza, walirudishe haraka kwa serikali ya kijiji ili lipangiwe matumizi mengine.

Agizo hilo amelitoa leo wakati akiwa njiani kuelekea Tanga kwa ajili ya kumpokea Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambapo kesho wataweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Kaskazini mwa Tanga.

Rais Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa wawekezaji au taasisi itakayopewa eneo kwa ajili ya kujenga kiwanda lazima ifanye hivyo, kushikilia eneo bila kuliendeleza kutasababisha mhusika anyang’anywe eneo hilo na apewe mwingine mwenye uwezo wa kuliendeleza.

Pia rais ametoa onyo kwa viongozi waliohusika kuhujumu kwa kujinufaisha na fedha kiasi cha Tsh milioni 500 za ujenzi wa Hospitali ya Mkata kuwa wajiandae kuzirudisha ama kwenda gerezani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *