Muigizaji wa Bollywood, Priyanka Chopra amekosolewa na watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa kuamua kuvaa gauni linaloonyesha miguu yake alipokutana na waziri mkuu wa India, Narendra Modi.
Baadhi ya watumiaji wa Facebook walimwambia kuwa alimkosea heshma waziri mkuu kutokana na kuvaa gauni fupi linaloonyesha miguu yake.
Mashabiki hao katika mtandao wa kijamii wamemwambia angepaswa kufunika miguu yake mbele ya waziri mkuu.
Mchezaji filamu huyo ambaye hakuomba msamaha alijibu kauli hizo za ukosoaji kwa kutuma picha akiwa na mama yake wote wakiwa wamevalia gauni fupi, yenye maandishi.
Wachezaji filamu wengine wa India pia wamekuwa wakilengwa na hasira za wakosoaji wa mavazi wanayochagua kuyavaa.
Utata ulianza alipotuma picha akiwa na Bwana Modi, akimshukuru kwa kuchukua muda licha ya kuwa na ratiba ya shughuli nyingi kukutana naye mjini Berlin nchini Ujerumani.
Muigizaji huyo amesema kuwa hakufikiria hata hivyo kwamba gauni la kukosa heshima litakuwa mada ya mazungumzo, huku wengi wakitoa kauli zao juu ya vazi hili.