Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi miwili kwa kampuni ya Swissport Tanzania kuhakikisha inaboresha huduma.

Kampuni hiyo ya Swissport ambayo inashughulikia mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam imelalamikiwa kushuka kwa huduma zake katika uwanja huo.

Waziri Mbarawa amesema, kampuni hiyo imefanya kazi kwa muda mrefu katika uwanja huo na hivyo haiwezi kujulikana kama huduma zake ni nzuri au mbaya kwa kuwa hakuna wa kumpima naye.

Alisema hivi karibuni alipata ripoti iliyokuwa ikionesha kuwa huduma za kampuni hiyo hazikuwa nzuri na kwamba katika kipindi cha mwaka jana Wizara yake ilitoa leseni kwa kampuni nyingine ya Nas-Dar Airco ambayo hata hivyo hadi sasa haijaanza kazi.

Alisema tangu kampuni ya Nas- Dar Airco ipewe leseni haijafanya kazi uwanjani hapo na inawezekana kukawa na sababu mbili ambazo ni Swissport kuweka mazingira ambayo yanaifanya kampuni hiyo ishindwe kufanya kazi lakini pia kampuni kutokuwa na uwezo. Hata hivyo, alisema haiwezekani kupima uwezo wake wakati haijapata fursa ya kufanya kazi.

Amesema ni lazima kampuni hiyo ifanye kazi katika uwanja huo pamoja na watu wengine na kwamba kama walizoea kufanya hivyo si kwa wakati huu kwa kuwa hizi ni zama tofauti, hivyo lazima wafuate taratibu na kanuni zilizowekwa, vinginevyo akipewa leseni ya kampuni hiyo ataifuta.

Aidha Profesa Mbarawa amesema anaamini kuna makampuni mengi duniani yanayoweza kutoa huduma hizo na kwamba suala hilo halihusiani na moto uliowaka katika chumba cha kuhifadhia mizigo kinachosimamiwa na kampuni hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *