Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amesema matunda ya elimu mtandao hayajaonekana kwa kiwango kikubwa nchini kwa kuwa shule nyingi hazina maabara za kompyuta.

Waziri huyo amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa elimu mtandao na kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuboresha elimu hiyo.

Ameyasema hayo wakati akifunga kongamano la wadau wa elimu nchini, lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan.

Kongamano hilo lililenga kujadili changamoto na fursa za elimu na kutoa mapendekezo kwa serikali. Liliwahusisha wataalamu wa masuala ya elimu kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi pamoja na viongozi wa kisiasa, wakiwemo wabunge.

Amesema elimu ya mtandao haijawanufaisha wanafunzi wengi nchini na hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, shule chache ndizo zenye maabara za kompyuta na wanafunzi wengi bado hawawezi kupata machapisho ya elimu kwa mtandao.

Katika kukabiliana na tatizo hilo amesema Serikali itaendelea kuwahusisha wadau wa sekta binafsi na wengine kuhakikisha kuwa elimu ya mtandao inawanufaisha wanafunzi nchini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *