Serikali imeagiza kuwa viongozi wa zamani waliotajwa jana kuhusika na mikataba mibovu ya madini wasitoke nje ya mipaka ya Tanzania mpaka kupata kibali maalum kutoka Serikalini.
Waliozuiliwa ni Mawaziri, Wanasheria Wakuu wa Serikali na Manaibu wao, Wakurugenzi wa idara za mikataba, na Makamishna wa madini, wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini na watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa makampuni ya madini.
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambaye alisema kuwa, wote waliotajwa kuhusika katika kulisababishia taifa hasara kupitia sekta ya madini, hawaruhusiwi kutoka nje ya mipaka ya Tanzania isipokuwa kwa kibali maalum kutoka serikalini.
Agizo hilo limekuja ikiwa ni saa chache tangu Rais Magufuli alipoagiza kuwa, viongozi wote na watumishi mbalimbali waliohusika katika kusaini mikataba mibovu na kushiriki kwa namna yoyote ile, wahojiwe.
Miongoni mwa watakaoathiriwa na zuio hilo, ni pamoja na Maafisa wa TRA, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Andrew Chenge, Mwanyika, na Werema, Mkurugenzi Idara ya Mikataba, Mary Ndosi, Kamishna Dalali Peter Kafumu, Waziri Prof. Muhongo, Waziri Daniel Yona, Waziri Nazir Karamagi, Jaji Julius Malaba, Waziri William Ngeleja.
Awali Waziri Nchemba alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada alizozichukua katika kuhakikisha analinda rasilimali za wanyonge na kusema kuwa hakuna uzalendo kama huo.