Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo amejiuzulu uanachama wa ACT-Wazalendo baada ya kudai kwamba inamuwia vigumu kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya pande zote mbili, yaani kwenye chama na serikalini.
Katika barua ambayo Prof. Kitila amethibitisha kwamba ni ya kwake, ameeleza kwamba kwa kipindi cha miezi 6 ambacho amefanya kazi serikalini kama mtumishi amekumbwa na mazingira magumu katika chama hasa pale anaposifia vitu vinavyofanywa na serikali ambayo yeye ni mtumishi wake.
Prof. Mkumbo amesema ameona ni vigumu kuendelea na ukatibu mkuu na uanachama wake bila kukwaza viongozi wa chama, hivyo ili kuepuka mgongano wa wazi wa maslahi amemamua kung’atuka uanachama wake kuanzia leo Oktoba 9, 2017.
Aidha, Prof. Mkumbo amewashukuru viongozi wote wa chama kwa ushirikiano wa juu waliomuonyesha tangu walipoanzisha chama hicho mwaka 2014.