Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO), kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi ili kufikia malengo ya serikali.

Hayo ameyasema jana wakati akiongea na uongozi wa mamlaka hizo mbili jijini Dar es Salaam.

Profesa Mkumbo amesema kuwa licha ya ongezeko la upatikanaji wa maji, zipo changamoto kubwa kwa wananchi kutofikiwa na huduma, hivyo ni lazima mamlaka husika kuongeza kasi ya usambazaji wa miundombinu ya maji.

Mkumbo ametoa rai kwa wateja wote wa Dawasco zikiwemo taasisi za umma, kutii agizo la Rais Magufuli la kulipia huduma wanazopatiwa ili kuziwezesha mamlaka husika kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa uzalishaji wa maji umeongezeka kutoka lita za ujazo wa mita 160 milioni kwa siku hadi kufikia lita za ujazo mita 271milioni kwa siku ambazo ni sawa na asilimia 100.37% ya lengo la upatikanaji wa maji ambalo ni lita 270 milioni kwa siku.

Katika kuhakikisha inafikia azma ya kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi Dawasco inaendesha kampeni ijulikanayo kama “Mama Tua Ndoo ya Maji Kichwani Ndani ya Siku 90” ikiwa na lengo la kuwaunganisha na huduma ya maji wateja takribani 151,000.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *