Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama cha Wananchi (Cuf), imeandaa ajenda ya kumfikisha Profesa Ibrahim Lipumba mbele ya Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho ili ajieleze na kujitetea ni kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kitendo chake cha kuvamia ofisi akiwa na wafuasi wake na kusababisha uharibifu wa mali za chama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui kutokana na kitendo cha kuvamia Ofisi Kuu ya chama hicho iliyoko Buguruni, Dar es Salaam na kusababisha uharibifu wa mali, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kitakachofanyika kesho.

Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 12 (6), (7) na (16) ya Katiba ya Cuf ya mwaka 1992, toleo la mwaka 2014, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeandaa ajenda na kumfikisha Profesa Lipumba mbele ya Baraza hilo ili ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa mambo aliyoyafanya.

Katika hatua nyingine, Mazrui alisema kamati hiyo imekataa maoni na ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Fransis Mutungi.

Pia amesema baada ya kupitia maoni na ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini juu ya malalamiko yaliyowasilishwa katika ofisi yake na Profesa Lipumba na wanachama wenzake waliochukuliwa hatua za kinidhamu na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Kamati hiyo inakataa na kupinga kwa hoja thabiti ushauri na maoni yaliyopendekezwa na Msajili.

Vile vile amesema kamati hiyo inaendelea kusimamia uamuzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Agosti 21, mwaka huu uliokubali kujiuzulu kwa Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa Chama na uamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa uliofikiwa katika kikao chake cha Agosti 28 mwaka huu.

Aliongeza kwa kusema kuwa uamuzi huo ni wa kuwasimamisha uanachama Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya, Maftah Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha Kapasha, Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa, Haroub Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye.

Alimaliza kwa kusema Katiba ya Cuf haina kifungu chochote kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kupokea rufaa kuhusu uamuzi wa vikao vya chama wala kubatilisha uamuzi wa vikao hivyo.

Baada ya kupitia hoja 11, Jaji Mutungi alimrejesha katika wadhifa wake wa Uenyekiti Profesa Lipumba, hali iliyosababisha mchumi huyo kuingia ramsi juzi ofisini kwa chama hicho, Buguruni na kuzua tafrani kutoka kwa wanachama wanaompinga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *