Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kurudi katika meza ya mazungumzo na kumaliza tofauti zao.

Lipumba amesema hayo leo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa chama hicho.

Mwenyekiti huyo amemtaka Katibu Mkuu huyo kurudi wafanye mazungumzo na atambue kuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa CUF na ndiye boss wake.

Amesema kuwa Maalim ni mkongwe katika siasa hivyo ni vyema kukawa na maelewano ili kazi za chama zisonge mbele katika kukiimarisha chama cha wananchi CUF ili kuweza kurudisha umoja na mshkamano waliokuwa nao.

Aidha, Prof.  Lipumba amesema kuwa kama Katibu Mkuu wa CUF ataendelea na kutotimiza wajibu wake wa kufika ofisini kwa ajili ya majadiliano na mazungumzo kwa lengo la kumaliza migogoro yao basi Naibu Katibu Mkuu ataendelea kukaimu nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba yao ya CUF.

Hata hivyo, Lipumba amekipiga dongo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) toka kimempokea, Edward Lowassa wameacha ajenda ya ufisadi na wameiweka kando ajenda hiyo na kusema sasa hivi wao ndiyo ajenda yao hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *