Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha kuwa asilimia 86.6 ya Watanzania hawajasajiliwa na hivyo hawana vyeti vya kuzaliwa.

Aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akifungua kikao cha wadau wa usanifu wa mpango wa usajili wa matukio ya binadamu.

Alisema takwimu hizo zinaonesha kwamba Watanzania asilimia 13.4 ndio wamesajiliwa na wana vyeti vya kuzaliwa. “Hii ni idadi ndogo na ni kiashiria kuwa serikali haina taarifa za idadi kubwa ya wananchi,” alisema Profesa Kabudi.

Pamoja na takwimu hizo, wapo wananchi ambao huzaliwa na kufa bila hata taarifa zao kuonekana katika kumbukumbu zozote za serikali. “Hali ya usajili wa matukio ya vifo, ndoa na talaka nayo hairidhishi pamoja na ukweli kwamba takwimu zake ni za muhimu kwa serikali,” alisema. Profesa Kabudi alisema serikali imeamua kufanya maboresho ya mfumo wa usajili uliopo kwa kuanzisha mfumo utakaofanya kazi vizuri wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu (CRVS).

Alisema mchakato wa kurekebisha mfumo wa sheria zinazosimamia masuala ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu umeshaanza.

Pia alipongeza Tume ya Kurebisha Sheria kwa kukamilisha utafiti na kufanya kwa kisayansi na kwa makini ukubwa na hivyo mwishoni mwa mwaka kutakuwa na mfumo wa kisheria uliorekebishwa.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA, Profesa Hamis Dihenga alisema CRVS utawezesha kusajili matukio ya binadamu, lakini pia utajua sababu za vifo vinavyotokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *