Jumla ya watu sita wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi katika eneo la Mbezi kwa Yusuf Makondeni katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya amesema watuhumiwa hao waliuawa katika majibizano ya risasi na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha.

Mkondya amesema wamepata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna kikundi cha watu wenye silaha, wamejipanga kufanya tukio la ujambazi kwa kutumia silaha kwa mfanyabiashara aliyekuwa akitoka Benki ya Diamond Trust Bank (DTB.

Vile vile amesema baada ya kupata taarifa hizo, polisi waliweka mtego na majambazi hao wakitumia gari aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T970 DGZ rangi ya fedha, walionekana wakilifukuza gari la mfanyabiashara huyo, kisha kulipita na kumsimamisha kwa nguvu.

Pia amesema kutokana na hali hiyo, askari walianza kujibu mashambulizi na kuwaua majambazi hao na baada ya upekuzi, zilipatikana bastola mbili, moja ya kijeshi aina ya Chinese ikiwa na risasi moja ndani ya kasha la risasi; na nyingine aina ya Browning ikiwa imefutwa namba zake na maganda sita ya risasi yaliyookotwa katika eneo la tukio.

Miili ya watuhumiwa hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa majambazi hao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *