Jeshi la Polisi limesema limeanza kufanyia kazi maagizo waliyopatiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kumsaka mtu aliyemtolea bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Hayo yalisemwa Ijumaa hii na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso. Awali, Gazeti la Mwananchi lilimtafuta Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu, lakini simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyemtaka mwandishi amtafute Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ili atoe ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa agizo la Waziri Nchemba.

Alipopigiwa simu, Senso alijibu kwa ufupi kuwa wameanza kufanyia kazi agizo la Waziri Nchemba. “Sisi tumepokea maelezo ya waziri na tayari tumeanza kuyafanyia kazi, hilo ndilo ninaloweza kukwambia,” alisema.

Hali hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya polisi aliyevalia kiraia kumtishia bastola, Nape ambaye pia ni Mbunge wa Mtama (CCM).

Sambamba na hayo Waziri Nchemba alilaani kitendo hicho na kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchukua hatua.

Source: Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *