Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amesema kikosi chake kimerudi katika kiwango chake na sasa ni mwendo wa ushindi katika mechi zake zilizobaki.

Yanga ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mabao ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Obrey Chirwa, Simon Msuva na Donald Ngoma na la Mtibwa likifungwa na Haruna Chanongo. Huo ni ushindi wa kwanza kwa Yanga baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Stand United na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba katika mechi zilizopita.

Pluijm amesema kiwango walichoonesha wachezaji wake kama wataendelea nacho ni wazi kuwa wataikaribia Simba inayoongoza kileleni.

Amesema kikosi chake kilicheza vizuri na kwa ushirikiano uliowezesha kutumia vyema nafasi walizopata katika kufunga.

Ushindi wa Yanga umeisogeza nafasi moja kutoka nafasi ya tano hadi nne ikiishusha Mtibwa Sugar iliyokuwa ikishika nafasi ya tatu.

Yanga sasa imefikisha pointi 14 katika michezo saba iliyocheza, nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 15 katika michezo tisa iliyocheza, Stand United ikishika nafasi ya pili kwa pointi 19 katika michezo tisa na Simba inayoongoza kileleni kwa pointi 20 katika michezo minane iliyocheza.

Mchezo ujao Yanga inatarajiwa kucheza na Azam FC keshokutwa, mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kwani Azam imekuwa haifanyi vizuri kwenye mechi zake na imetoka kupoteza juzi ya Stand United, hivyo itataka kushinda.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *