Aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amesema milango iko wazi kwa timu yoyote inayomhitaji kufanya nae mazungumzo.

Kocha huyo Mholanzi alitangaza kujiuzulu baada ya waajiri wake Yanga kuingia mkataba na kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina bila kumshirikisha.

Licha ya kujiuzulu, taarifa za Yanga zilisema kuwa Pluijm alitakiwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na nafasi yake ya ukocha angepewa Lwandamina jambo ambalo Pluijm alilikataa.

Pluijm amekuwa akihusishwa na kujiunga na Azam FC jambo ambalo amelikanusha kuwa halina ukweli.

Amesema sio vyema kuzungumzia timu ambayo tayari ina makocha wake, kitaalamu haipendezi.

Kwa upande wa Azam FC walisema kwa sasa hawana mpango wa kumbadilisha kocha, kwani aliyepo bado ana mkataba, na kwamba wanaamini wachezaji watamuelewa taratibu falsafa yake na mambo yatakwenda vizuri.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema jana kuwa Pluijm ni kocha mzuri na anasikitika kuondolewa kwake katikati ya ligi na kwamba anamheshimu isipokuwa hawana mpango wa kumchukua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *